
Jeshi kamili la kikosi cha Simba linamekamilika kuelekea mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo itakayopigwa keshokuwa Jumapili Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya wachezaji watatu waliokuwa majeruhi kurejea kujifua na wenzao.
Simba iliwapoteza wachezaji wake watatu; kipa Aishi Manula, mshambuliaji Ibrahim Ajibu, na mshambuliaji Mbrazil Wilker Henrique da Silva waliokuwa majeruhi, lakini sasa wamerejea kikosini kujifua na wenzao.
Wakati wachezaji hao wakirejea, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu amesema kwamba chumba cha majeruhi amebaki nahodha John Bocco, ambaye aliumia wakati wakishinda 4-2 na kutwaa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki iliyopita.
“Ajibu, Manula na Wilker da Silva wamereja na wanajifua na wenzao, kilichobaki sasa ni uamuzi wa Kocha Mkuu Patrick Aussems, kuamua atampanga nani kuelekea mechi yetu ya marudiano Jumapili,” alisema Rweyemamu.
Hata hivyo, licha ya nyota hao kurejea kutokana na ubora wa kila mchezaji anayepata nafasi kuonyesha uwezo mkubwa, Aussems atalazimika kuchanga karata yake vizuri ya nani aanze katika kikosi hicho.
Kipa Beno Kakolanya, ameonyesha ubora wa hali ya juu tangu alipoanza kuidakia timu hiyo dhidi ya Power Dyanamos kwenye mechi ya Simba Day na kuiongoza kushinda 3-1, kisha wakatoka sare tasa dhidi ya UD Songo ugenini kabla ya kuiongoza kushinda 4-2 dhidi ya Azam FC kwenye Ngao ya Jamii.
Ni wazi, Manula anaweza kusubiri kwa muda kabla ya kumshawishi Aussems hasa ukizingatia anahitaji kujiweka fiti zaidi kutokana na kutokea chumba cha majeruhi, lakini pia Ajibu na Da Silva wana kazi ya kufanya katika nafasi zao.
Ajibu na Da Silva wanapaswa kuonyesha ubora wa hali ya juu wakati huu Bocco akiwa majeruhi, kwani tayari hakuna kati yao anayeweza kumweka benchi kwa sasa, Sharaf Eldin Shiboub ama Clatous Chama au hata Hassan Dilunga ‘HD’.
Upana wa kikosi cha Simba umeanza kuonekana mapema hususan idara ya kiungo mshambuliaji kutokana na uwezo mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji wa nafasi hizo.
Simba keshokutwa itahitaji ushindi wa aina yoyote ili kuweza kusonga mbele katika mchuano hiyo ambayo msimu uliopita iliishia robo fainali kufuatia kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo kwa jumla ya mabao 4-1.
Kama Simba itasonga mbele ama UD Songo, itakuna na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi ambayo kesho itakuwa ugenini ikisaka matokeo baada ya mechi ya awali kulazimishwa sare tasa nyumbani
Nipashe