
Baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Ethiopia jana kwenye mechi ya ufunguzi ya Michuano ya CECAFA U20 Challenge Cup inayoendelea nchini Uganda, timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Ngorongoro Heroes’ kesho itashuka dimbani kuikabili Kenya.
Mchezo huo ambao utaanza saa 7 mchana unatarajiwa kuwa mkali baada ya Kenya kuifunga Zanzibar mabao 5-0 katika mechi yake ya ufunguzi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha Fufa.
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Zubeiry Katwila amesema kwa namna alivyoitazama Kenya vijana wake wanatakiwa kucheza kwa kujituma zaidi ili kuweza kupata ushindi wa pili na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. “Tumewaona Kenya, ni timu nzuri. Uzuri ni kwamba hata wachezaji pia walikuwepo uwanjani na kuona wapinzani wetu wamefanya kitu gani. Utakuwa ni mchezo mzuri na wa ushindani, tunaimani timu yetu itafanya vizuri,” alisema Katwila.
Kwa upande wake beki wa kati wa timu hiyo, Oscar Masai, amesema tayari mwalimu wao amewapa mbinu sahihi za kuikabili Kenya hapo kesho, huku akisisitiza kuwa hali ya wachezaji ni nzuri na wamejipanga kushindana. “Kama wachezaji tuko vizuri, tunashukuru kwamba tulianza mechi ya kwanza kwa matokeo bora, tunatamani kuendeleza hicho. Kuhusu Kenya, Mwalimu aliwaona vizuri na ametuambia nini cha kufanya hapo kesho,” alisema Masai ambaye ni mchezaji wa Azam FC.
Naye straika wa timu hiyo, Andrew Simchimba aliyefunga mabao matatu ‘Hat Trick’ kwenye mechi dhidi ya Ethiopia, amesema anatamani kuendelea na kiwango chake bora alichoanza nacho katika mashindano hayo ili kuweza kuisaidia timu.
@tanfootball @serengetiboystz
Credit : @giftmacha_official
#wapedasokaupdates













