
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba ambao ndio vinara wa ligi kuu, leo wanaanza mzunguko wa pili wa Ligi hiyo kwa kuwakaribisha ‘Maafande’ wa JKT Tanzania katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi mfululizo wa mechi tano wakati JKT Tanzania wao wametoka kubanwa nyumbani kwa kulazimishwa sare dhidi ya Coastal Union kutoka jijini Tanga.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema kikosi kiko tayari na kamili kwa mchezo huo na kuitaja JKT Tanzania ni moja ya timu zenye wachezaji walioimarika na wenye kutoa ushindani kwa klabu pinzani.
Matola alisema wamewaandaa wachezaji wao kupambana katika mechi zote kwa sababu hatua ya lala salama ndio wakati wa kukamilisha ‘hesabu’ za ubingwa.
Alisema hakuna mechi rahisi na hakuna timu ndogo katika Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo watakuwa makini katika kila mpira watakaokuwa nao wachezaji wake.
“Ni mechi ngumu, hatutarajii kitu kingine, msimu huu na hasa mzunguko huu mambo yatazidi kuwa magumu, kila timu inahitaji kukamilisha malengo yake, bado hakuna ambaye yuko salama, walioko chini wanataka kukimbia na walioko chini yetu wanatukimbiza,” Matola alisema.
Nahodha na kiungo huyo wa zamani wa Supersport ya Afrika Kusini alisema wanahitaji kuendeleza matokeo mazuri katika kila mechi ili watangaze ubingwa mapema.
“Hatutaki presha huko mbele, ukifanikiwa kushinda mechi nyingine tano za mzunguko wa kwanza, unakuwa nafasi salama, dua na mipango yetu ni kutoangusha pointi katika mechi hizi za nyumbani, tumejiandaa kukabiliana na kila ushindani,” alisema Matola.
Naye Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wachezaji wote wapo salama na wanaendelea kujipanga kwa ajili ya mechi hiyo ya leo.
“Tuliendelea na mazoezi kama kawaida, kama unavyojua kwa sasa huwezi kufanya mazoezi magumu, mwalimu huangalia na kuwapa mbinu zake za kiufundi baada ya kurekebisha makosa ya mchezo uliopita, tuko vizuri, tunaamini tuna nafasi ya kupata pointi tatu nyingine,” alisema Rweyemamu.
Aliongeza kuwa nyota wao wawili, Shiza Kichuya pamoja na Luis Miquissone, tayari wamepata ITC na uwezekano wa kuonekana uwanjani leo utatokana na uamuzi wa Kocha Mkuu Mbelgiji Sven Vandenbroeck.
Baada ya mechi ya leo, Simba itasafiri kwenda Morogoro kuwafuata Mtibwa Sugar katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa Jumanne na Februari 15, mwaka huu watakuwa ugenini Iringa kuwakabili Lipuli FC kwenye Uwanja wa CCM Samora mkoani humo.