
Nyota wa zamani wa klabu ya Simba Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ amesema moja ya sababu iliyopelekea Simba kuondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa, ni kitendo cha kuidharau UD Songo
Julio ambaye pia amewahi kuwa kocha wa Simba, amesema baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa ugenini, pamoja na mafanikio iliyopata Simba kwenye michuano hiyo msimu uliopita, wachezaji waliona watakuwa na kazi rahisi
“Wachezaji walijisahau, baada ya kupata suluhu ugenini kwenye mchezo wa kwanza. Lakini pia wengine wakachukulia mambo yataenda tu kama walivyofanya msimu uliopita,” amesema
“Waliuanza mchezo taratibu wakati wenzao walianza kwa kasi wakihitaji kufunga bao la ugenini ambalo mwisho wa siku limewavusha”
Awaponda Wabrazil
Julio, kocha mwenye maneno mengi pia ameponda usajili wa wachezaji watatu kutoka Brazil akiwatuhumu waliofanikisha usajili huo kuwa wamehujumu fedha za Mo
“Hakuna mbrazili anayeweza kuja kucheza soka Tanzania”
“Watu wa huko wana malengo ya kucheza soka la mbele zaidi, hao wamekuja kutalii tu na si wachezaji mpira, subirini mtaona”
Awali ilielezwa kuwa wachezaji hao walisajiliwa kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa hata hivyo ni Fraga pekee aliyepata nafasi ya kucheza kwa dakika chache mchezo wa kwanza dhidi ya UD Songo
Mshambuliaji Wilker Da Silva bado ni majeruhi huku beki Tairone Santos yeye akishiriki mechi moja tu Simba Day
Hata hivyo kocha Patrick Aussems alieleza sababu ya kutowatumia wachezaji hao akisema bado wanahitaji kujifunza utamaduni wa soka la Afrika
Aidha amesema suala la lugha pia ni tatizo linalowafanya wachelewe kuzoea mazingira
Lakini alisema wameonyesha viwango vizuri, na watapewa nafasi kulingana na mahitaji ya mchezo