
Siku chache tangu uongozi wa klabu ya Simba kumtambulisha bosi mpya, kitendo hicho kimelipandisha mzuka benchi la ufundi ambalo limeapa kukisuka zaidi kikosi ili kiwe na makali ya kufanya mauaji katika mechi zao zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wikiendi iliyopita, Simba walimtambulisha rasmi Senzo Mazingisa, raia wa Afrika Kusini, kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (C.E.O) baada ya Crescentius Magori, kumaliza muda wake.
Moja ya vitu ambavyo Mazingisa, alivyovingumza katika utambulisho wake, ni kuifanya Simba kuwa klabu bora Afrika kulingana na makubaliano ya mkataba wao.
Kauli hiyo ya Mazingisa inaonekana kuanza kufanyiwa kazi na benchi la ufundi ambalo linataka kusuka kikosi cha maangamizi kuelekea mechi zao za Ligi Kuu Bara na michuano yoyote itakayopita mbele yao.
Katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam, inadhihirisha hilo kwa sababu ya aina ya tizi walilokuwa wanapewa wachezaji wa timu hiyo.
Licha ya uwepo wa wachezaji wachache mazoezini kutokana na wengine kuwa na majukumu ya timu zao za Taifa, Kocha Mkuu Patrick Aussems, alikuwa makini kuhakikisha kila mmoja anafanya kile anachotaka.
Wekundu wa Msimbazi hao, walikuwa wakifanya mazoezi ya aina tofauti, zaidi ikiwa yale ya kuongeza pumzi na kasi ya kukimbia wanapokuwa uwanjani.
Wacheza walikuwa wanakimbia kwa zamu huku wamefunga vifaa vya kuwafanya kuwa na kazi pamoja na pumzi, kocha akiwa amewasimamia, wakipokezana.
Kocha Patrick Aussems, aliweka bayana kuwa lengo kwa sasa baada ya kupitia kipindi kigumu cha kuondolewa katika michuano ya kimataifa, anataka kuwadhihirishia wapenzi wa soka kuwa kikosi chao ni bora.
Aussems alisema kutokana na maandalizi wanayofanya, ubora wao utaanza kuonekana katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar inayotarajia kuchezwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Alisema mechi yao imerudishwa nyuma, tofauti na simu waliyotakiwa kucheza, lakini hilo halimpi presha kwani msimu huu wamejipanga na kitendo cha ratiba hiyo kubadilika hakijaathiri chochote.
“Tumeendelea na mazoezi kwa wachezaji ambao hawapo katika timu za Taifa, nafurahi kikosi kipo vizuri tumejipanga kukabiliana na Mtibwa Sugar, tena imerudishwa tunacheza Ijumaa, hiyo haina tatizo.
“Haya mazoezi ya mbio tuliyoyafanya leo(jana), ni kuwaweka wachezaji vizuri, mengine yamepita na sasa tunaangalia mbele kuonyesha kila mtu kwamba sisi ni timu bora na hilo litaanzia siku ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar,” alisema Aussems.
BINGWA