
Uongozi wa klabu ya Yanga umesema umeipokea kwa furaha droo ya mtoano wa michuano ya kombe la Shirikisho wakiwa wamepangwa kucheza na Pyramids Fc ya Misri
Akizungumza baada ya droo hiyo iliyofanyika jana nchini Misri, Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema wanazo taarifa za kutosha kuhusu mpinzani wao na wameanza rasmi maandalizi kuelekea mchezo huo
“Tunafahamu ni timu iliyoanzishwa mwaka 2008. Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya tatu ligi kuu ya Misri na hivyo kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho,” amesema
“Pia tunafahamu katika mechi zao nne za kombe la Shirikisho mpaka kufika hatua hii, wameshinda mechi mbili ugenini, sare na ushindi nyumbani”
“Ni timu yenye utajiri mkubwa, mapema mwaka huu tunafahamu ilinunuliwa na matajiri kutoka Arabuni”
“Lakini hilo halitutishi Yanga kwa sababu tunafahamu hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano ya Kimataifa”
“Miaka ya hivi karibuni tumecheza Misri na vilabu vya Al Ahly na Zamalek na tulitoa ushindani mkali. Hivyo sisi hatuzihofii kabisa timu kutoka Misri”
“Kwa sababu tumeshamfahamu mpinzani wetu, tutaboresha ratiba yetu ya maandalizi ili kuhakikisha tunakuwa tayari kupata ushindi kwenye mchezo wa nyumba ambao utapigwa Oktoba 27”
Pyramids Fc inakadiriwa kuwa na kikosi chenye thamani ya zaidi ya Bil 60, ikinolewa na kocha wa zamani wa Uganda Cranes Sebastiane Desabre ambaye aliipeleka Uganda Misri kwenye michuano ya Afcon 2019
Pamoja na timu hiyo kuwa ngeni, uwekezaji mkubwa uliowekwa ni ishara kuwa wanataka mafanikio ya haraka kwenye soka la Afrika
Ukingalia klabu hiyo imeanzishwa mwaka 2008 na mwaka jana ilibadilishwa jina na kuitwa Pyramids Fc
Ndani ya msimu mmoja matajiri wametumia zaidi ya Tsh Bilioni 60 kuunda kikosi
Hapa Yanga lazima ifanye maandalizi ya kutosha na muhimu zaidi ni kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wao wa nyumbani kwani ni kawaida timu za Misri zinapokuwa kwao ni ngumu kufungika