
ABDULAH MKEYENGE
NAPENDA kumtazama kiungo Mbrazil wa Simba Gelson Fraga. Ni kiungo anayejua kutimiza vyema majukumu yake. Mpira ukiwa mguuni mwake hakai nao hata kwa sekunde kumi anautoa kuupeleka kwingine. Viungo wa kileo ndiyo wanacheza hivi.
Kuna sehemu tunajidhulumu tunapomtazama Fraga, kibaya zaidi tumeamua kumdhulumu na Fraga mwenyewe. Tunamtaka afanye zaidi ya anachotuonyesha. Kiungo wa chini hapaswi kuwa na mambo mengi mguuni. Kwake mpira unatakiwa kuwa njia kuelekea kwa mtu mwingine.
Ubrazil wa Fraga unamuhukumu mbele ya mboni zetu. Tunapoambiwa mchezaji anatokea Brazil, picha ya kwanza inayotujia ni Ronaldinho Gaucho.
Tunamtaka Fraga awe kama Gaucho. Amekuja na aina nyingine ya mchezo tunamuona mchezaji wa hovyo asiyestahili kuvaa jezi ya Simba. Watanzania tumechelewa kujua mpira, mbaya zaidi hatutaki kujifunza mpira wenyewe ulivyo. Tukiwa na msimamo wetu ni ngumu kutubadili.
Fraga anacheza basic football. Haupandi mpira, hampigi mtu tobo, kanzu. Mchezaji aliyepitia academy katika eneo lake anatakiwa acheze vile anavyocheza. Namba sita si sehemu ya kuuchezea sana mpira. Si sehemu salama mpira ukipotea.
Ubrazil wa Fraga umefanya tutake kumsuta. Tuna lundo la maswali kila tunapomtazama. Swali letu kuu inakuwaje Fraga hana udambwi kama Ajib ambaye ni Mtanzania mwenzetu? Hili ni swali tunalolijiuliza kila leo. Tumekwamia hapa.
Hatumtazami kiufundi. Tumebaki kumuhukumu na uraia wake. Usipomtazama Fraga kiufundi unaweza usilione jukumu lake kiwanjani kutokana na kukosa mboga mboga mguuni mwake.
Fraga anawafanya walinzi wa Simba wawe salama. Hatembei eneo kubwa. Anachokifanya ni kusimama mbele ya mabeki wanne na kuwalinda.
Unamuona Mbwana Samatta dhidi ya Wazungu? Anawatesa Wazungu kadri anavyojisikia. Lakini Wazungu wanamfurahia na kuushangaa Utanzania wake. Wengi walidhani anatokea Afrika Magharibi au Kaskazini. Hawaamini kama katoka Tanzania.
Garry Lineker jana katikati ya wachambuzi wake studio (Peter Crouch, Rio Ferdinand, Robin Van Parsie) alimshangaa Mbwana kama sisi tunavyomshanga Fraga. Hajamshangaa kwa ubaya.
Tofauti ya Lineker na sisi ni kwamba, Lineker ameshangazwa na kiwango cha Mbwana. Sisi hatuishii kumshangaa Fraga, pia tunamuona hana analolijua kabisa. Tumechelewa kujua mpira.
Katika nchi ambayo haijawahi kushinda Kombe la Mataifa Afrika, haijawahi kufuzu Kombe la Dunia wala kukaribia kufuzu, mashabiki wa nchi yake wanatoa wapi ujasiri wa kutambua mchezaji bora?
Muda huu tunaomshangaa Mbrazil Fraga kwa kumuona hajui, wacha Wazungu waendelee kuufurahia ubora wa Mtanzania Samatta.


.


#TanzaniaVodacomPrimierLeague
#TanzaniaVodacomPrimierLeague

